Kampeni ya Elimu ya Nishati Safi ya Kupikia na Uhifadhi wa Mazingira Yaibua Mwanga Mpya kwa Jamii ya Muungoni
MIF kwa kushirikiana na Pamoja Youth Initiatives imeendesha kampeni ya elimu kuhusu nishati safi ya kupikia na uhifadhi wa mazingira katika Shehia ya Muungoni, kwa lengo la kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ambayo ni salama kwa afya, rafiki kwa mazingira na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi. Wananchi walipata elimu kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa nishati safi ya kupikia, ikiwemo uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya teknolojia za nishati safi. Kampeni hii iliwakutanisha wadau mbalimbali waliotoa elimu na uzoefu katika maeneo tofauti. ORYX ilitoa elimu kuhusu matumizi salama na sahihi ya gesi ya kupikia, Samia Foundation ilitoa elimu ya lishe bora na umuhimu wake katika kuboresha afya za jamii, huku Mpishi Hodari akitoa elimu na maonesho ya matumizi ya nishati safi pamoja na majiko yanayotumia umeme mdogo, yanayosaidia kupunguza gharama za kupikia na kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati majumbani. Mkutano huo ulihudhuriwa na wanajamii zaidi ya 280, jambo linaloonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kupokea elimu inayolenga kuboresha afya, kulinda mazingira, kupunguza umasikini na kufungua fursa za kiuchumi kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa pamoja tunaendelea kujenga jamii yenye afya bora, mazingira salama na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.