MIF YAHITIMISHA MAFUNZO YA SIKU TANO YA UOKAJI KWA WANAWAKE NA VIJANA
Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) imehitimisha kwa mafanikio mafunzo ya siku tano ya uokaji yaliyolenga kuwawezesha wanawake na vijana kupata ujuzi wa vitendo utakaowasaidia kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya jamii.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na mkufunzi Alexander's Cake, ambaye aliwapa washiriki maarifa ya kina kuhusu mbinu za kisasa za uokaji pamoja na misingi ya kuanzisha na kuendesha biashara ndogo zinazotokana na ujuzi huo.
Akizungumza wakati wa mahafali ya wahitimu, Mwenyekiti wa Mwanamke Initiatives Foundation, Mhe. Wanu Hafidh Ameir Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia aliwapongeza washiriki kwa kujituma katika kipindi chote cha mafunzo na kuwahimiza kutumia ujuzi walioupata kama nyenzo ya kujenga uchumi wao binafsi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa ZEEA, ambaye alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali katika kuwawezesha wanawake na vijana kupitia mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali.
Mwanamke Initiatives Foundation inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwawezesha wanawake, vijana na makundi yenye uhitaji kupitia elimu, maendeleo ya kiuchumi, afya na ujenzi wa uwezo. Kupitia programu kama hizi, MIF inaamini kuwa ujuzi wa vitendo ni msingi muhimu wa kujenga jamii inayojitegemea na yenye ustawi endelevu.